Mabasi yaliyo andaliwa na JWTZ kukabili mgomo yako wapi?

May 5, 2015

“KUTOKANA na mgomo wa madereva wa mabasi ya abiria nchi nzima uliofanyika Ijumaa iliyopita, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilikuwa limeshaandaa mabasi 300 ambayo yangetumika kusafirisha abiria, imebainika.

Chanzo cha habari kutoka serikalini kimebainisha kuwa JWTZ ilikuwa imeweka tayari mabasi hayo na kuwa walikuwa wakisubiri taratibu za kufanya kazi hiyo, ikiwa ni pamoja na kujua safari za mabasi hayo na nauli ambayo wangewatoza wananchi.

Taarifa za ndani zinabainisha kuwa mgomo wa madereva wa abiria ulipangwa kufanyika kwa zaidi ya siku mbili, jambo ambalo lilifanya serikali kuliandaa jeshi kuwa tayari kutoa huduma kwa wananchi.

Ijumaa iliyopita, mamia ya abiria katika maeneo mengi ya nchi walipata madhila na mahangaiko baada ya madereva wa mabasi ya abiria nchi nzima kugoma, wakishinikiza serikali kubadili masharti ya kutakiwa kusoma kila wanaposajili leseni zao za udereva kila baada ya miaka mitatu, na matumizi ya tochi barabarani unaofanywa na askari wa usalama barabarani.

“Mbali na kulinda mipaka ya nchi kutoka kwa maadui wa nje, jeshi pia lina wajibu wa kuimarisha amani na usalama, na pia kufanya shughuli za kijamii kama vile kuingilia na kutoa huduma fulani muda wowote wanapotakiwa kufanya hivyo na serikali,” ilibainika.

Huu ni ushahidi kwani JWTZ imekuwa ikishiriki kusaidia jamii katika masuala mbalimbali wanapohitajika, ikiwa ni pamoja na kutumia vifaa vyao kujenga madaraja ya dharura, kuokoa maisha ya watu na kutolea mfano wa mafuriko ya Jangwani mwaka 2011 ambapo Jeshi lilishiriki katika kuwaokoa watu waliokuwa wamekwamba kwenye nyumba zilizokuwa zimezingirwa na maji.

Chanzo cha habari kimebainisha kuwa Jeshi lina mabasi mengi, na kutoa mfano tukio la hivi karibuni nchini Malawi wakati Rais Peter Mutharika alipotangaza hali ya hatari, JWTZ ilitoa malori 46 yaliyotumika kusafirisha msaada wa mahindi na dawa kwenda Malawi.

Kwa mujibu wa Nyasa Times, Serikali ya Tanzania ilichangia tani 1,200 za mahindi na dawa za binadamu katika kuisaidia serikali ya Malawi kupunguza uhaba wa chakula na magonjwa miongoni mwa maelfu ya Wamalawi kutokana na mafuriko ambayo yaliikumba nchi hiyo. Msaada huo ulikabidhiwa kwa Malawi na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Patrick Tsere.

Mgomo wa maderva wa mabasi ya abiria ya mikoani na baadhi ya mabasi ya Usafiri Dar es Salaam maarufu kama daladala uliibua vurugu katika kituo cha mabasi ya kwenda mikoani, hali iliyolazimisha askari Polisi kutumia mabomu ya machozi kurejesha hali ya amani”

Source| Habari leo 14/04/2015

Advertisements

BARAZA LA MTIHANI LATOA UFAFANUZI WA GRADE NA ALAMA ZA MATOKEO YA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE 2013

February 26, 2014

baraza

UFAFANUZI WA MASWALI MBALIMBALI YA WADAU WA ELIMU KUHUSU MATOKEO YA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE (CSEE) 2013

Baraza la Mitihani la Tanzania lilitangaza matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) 2013 tarehe 21/02/2014. Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Baraza limekuwa likipokea maswali mbalimbali yanayoashiria kuwa baadhi ya wadau wa elimu hawakuelewa vizuri kuhusu Viwango vya Ufaulu (grade ranges), alama ya chini ya ufaulu (pass mark) na Ufaulu wa jumla wa mtahiniwa (overall performance). Baraza la Mitihani linapenda kutoa ufafanuzi katika mambo hayo kama ifuatavyo:

  • Viwango vya ufaulu (grade ranges) ni makundi ya alama yanayopangwa ili kuwaweka pamoja watahiniwa wenye uwezo unaofanana katika somo husika na kuwatofautisha na watahiniwa waliopo katika kundi jingine. Makundi haya hupangwa ili kuwawezesha wadau kutambua namna watahiniwa walivyotawanyika katika viwango mbalimbali vya umahiri wa somo husika. Baraza la Mitihani la Tanzania, limekuwa likitumia makundi Matano (5) kwa kipindi kirefu hadi mwaka 2012. Aidha, Kuanzia Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) 2013, Baraza limeanza kutumia utaratibu wa Makundi Saba (7) ambayo ni A, B+, B, C, D, E na F. Utaratibu huu umelenga kupunguza mlundikano mkubwa wa alama katika kundi moja. Mgawanyo wa makundi hayo ni kama inavyoonekana kwenye Jedwali la 1.

 

Jedwali Na 1: Viwango vya ufaulu vilivyotumika katika Matokeo ya CSEE 2013.

Kundi

Gredi

Alama

Idadi ya Pointi

1

A

75 – 100

1

2

B+

60 – 74

2

3

B

50 – 59

3

4

C

40 – 49

4

5

D

30 – 39

5

6

E

20 – 29

6

7

F

0 –  19

7

Aidha, Idadi ya makundi ya ufaulu hutofautiana kati ya nchi na nchi kulingana na mahitaji ya nchi husika.  Kwa mfano; Kenya wana makundi Kumi na mbili (12), Malawi Tisa (9), Uganda Tisa (9), Nchi za Afrika magharibi (Nigeria, Ghana, Siera Leone na Liberia) makundi Tisa.

  • Kwa kuzingatia viwango vya ufaulu vilivyoainishwa katika makundi saba yaliyopo kwenye Jedwali na 1, kiwango cha chini cha ufaulu ni gredi D na kiwango cha juu cha ufaulu ni Gredi A. Mtahiniwa atakuwa amefaulu somo husika iwapo atapata gredi D na kuendelea. Aidha, mtahiniwa aliyepata gredi E na F atakuwa hajafaulu somo husika.
  •  Madaraja ya ufaulu yamepangwa kwa mujibu wa kifungu cha 20 (1)-(6) cha Kanuni za Mitihani kinachoelekeza kuwa Ufaulu katika daraja la Kwanza hadi la Tatu upangwe kwa kuzingatia jumla ya alama (Points) na Ufaulu katika Daraja la Nne unapangwa kwa kuzingatia ufaulu wa chini aliopata mtahiniwa ambao ni gredi D katika masomo yasiyopungua mawili au ufaulu kwa kiwango kisichokuwa chini ya Gredi C katika somo moja. Hivyo, madaraja yaliyotumika ni kama yanavyoonekana kwenye Jedwali la 2.

Jedwali 2: Madaraja yaliyotumika katika CSEE 2013

Daraja

Pointi

I

7 – 17

II

18 – 24

III

25 – 31

IV

  1. Ufaulu katika somo moja kwa kiwango kisichokuwa chini ya Gredi C au
  2. Ufaulu katika masomo yasiyopungua mawili katika Gredi D

0

Alama chini ya D mbili
  • Kwa mujibu wa Kanuni za Mitihani, ufaulu wa somo katika Gredi A hadi C utakuwa ni ufaulu wa “Credit” na Gredi D itahesabika kuwa ni “pass”. Aidha Gredi E na F zitakuwa alama za kufeli.
  • Baraza la mitihani la Tanzania linapenda kutoa taarifa kwamba ufafanuzi wa sifa za kujiunga na mafunzo katika ngazi mbalimbali kwa kutumia mfumo huu mpya wa madaraja utatolewa na mamlaka husika ambapo Kamishna wa Elimu atalitolea ufafanuzi zaidi.

 Imetolewa Na:

KAIMU KATIBU MTENDAJI


MAdhara ya kuvaa nguo za kubana (SKIN TIGHT)

February 25, 2014

Nguo za kubana

KIM KARDASHIAN - SKIN TIGHT RACING SUIT - 8

KADIRI siku zinavyokwenda kumekuwapo na ugunduzi wa vitu mbalimbali vinavyochangia kuleta mabadiliko katika jamii. Mabadiliko hayo yanaweza kuwa hasi au chanya kutegemea na aina ya bidhaa iliyogunduliwa na matumizi yake. Zipo bidhaa zinazoonekana kuwa na matokeo ya haraka na mazuri baada ya kutumika, lakini wakati huo huo kuwa na madhara kiafya kwa mtumiaji. Nchi nyingi zinazoendelea hasa zilizopo barani Afrika ikiwamo Tanzania zimekuwa ndizo waathirika wakubwa wa bidhaa zinaotajwa kuwa na madhara huku vijana wakiwa ndiyo kundi kubwa linaloathirika. Sababu za kundi hilo kuathirika zaidi ni kutaka kwenda na wakati kwa kujaribu kutumia kila bidhaa zinazotoka nje ya nchi bila kujua madhara yake. Miongoni mwa bidhaa hizo ni nguo za ndani zilizoundwa maalumu kwa ajili ya kupunguza unene, pia kutengeneza umbile la mvaaji katika mwonekano wenye mvuto aupendao. Nguo hizo zimetengenezwa kwa mtindo wa mbano, (Skin tight)ambapo ikivaliwa hubana eneo la tumboni hadi kwenye mapaja na hufanya kazi ya kupunguza unene, zikiufanya mwili kuwa mwembamba kulingana na nguo husika ilivyo. Licha ya kufanya kazi hiyo kwa ufanisi na kusaidia kwa kiasi kikubwa watu wengi kupunguza miili yao, utafiti wa kisayansi unaonyesha kuwa nguo hizo za ndani huchangia kwa kiwango kikubwa uwezekano wa mvaaji kupata matatizo ya kiafya. Utafiti uliofanywa na wataalamu mbalimbali wa nchini Uingereza, unaonyesha kuwa uvaaji wa nguo hizo unaweza kumfanya mvaaji kupata maradhi ya mgongo, saratani na kiwango kikubwa cha asidi mwilini. Mmoja wa wataalamu wa afya katika Hospitali ya The London Clinic, Dk Johnson Wilson, anasema kubana kwa nguo hizo katika eneo la tumbo huzuia mzunguko wa asidi inayozalishwa ndani ya mwili na kuisababisha kupanda juu, badala ya kushuka chini. Anasema kuwa hali hiyo inatokana na msukomo unaotokea kwenye tumbo, hivyo kusababisha mlundikano wa asidi ndani ya mwili ambayo hupaswa kutoka baada ya kuzalishwa. “Nguo hii inapovaliwa inatenganisha eneo la kifuani na tumbo, hivyo asidi inayozalishwa inashindwa kushuka chini na matokeo yake inashia kwenya usawa wa matiti na kurudi kwenye mrija unaopitisha chakula,”anasema DkWilson. Kuhusu hatari ya saratani, Dk Wilson anasema kuwa kulundikana kwa asidi katika mrija wa chakula, kunamweka mhusika katika hatari ya kupata saratani ya koo na kinywa. Anasema kwamba licha ya kuwa siyo watu wengi walioathirika na uvaaji wa nguo hizo, lakini matokea yake huonekana baada ya muda mrefu kutokana muda ambao mhusika atavaa nguo hizo. “Hatari ipo zaidi kwa wanaovaa nguo hizi mara kwa mara, madhara yake hayawezi kuonekana kwa haraka zaidi, lakini kiafya kuna hatari ya kutengeneza saratani ya koo kutokana na kuzuia asidi na kusababishia irudi na kulundikana kwenye mrija unaosafirisha chakula,”anaonya. Pamoja na hatari hiyo uvaaji wa nguo hizoi pia unachangia kusababisha ugonjwa wa ngozi unaotokana na mwili kubanwa kupita kiasi, hivyo hewa kushindwa kupita. Dk Wilson anafafanua kuwa ikifikia hatua hiyo, kuna uwezekano wa kutengeneza mazingira ya bakteria na fangasi kujificha kwenye mwili hivyo kusababisha mvaaji kupata maradhi ya ngozi yaliyo magumu kutibika. Mtaalamu wa ngozi Dk Sam Bunting anasema, kubanwa kwa ngozi pamoja na joto linalosababishwa na msuguano, vinachangia kuleta madhara makubwa katika mwili wa binadamu. “Hali hii inasababisha ugonjwa unaofahamika kwa jina la kitaalamu kama Intertirgo, ambao huwatokea watu wanaovaa nguo maalumu za kubana kwa ajili ya kutengeneza maumbile,”anasema. Nguo hizo pia huchangia kuifanya misuli ya tumbo kuwa dhaifu, kutokana na kubanwa muda mwingi, hata inapoachwa huru inashindwa kuwa na nguvu yake ya kawaida. “Kwa asili misuli ya tumbo haina nguvu na unapoibana kwa muda mrefu unaisababishia kushindwa kufanya kazi yake kwa ufanisi, hivyo hulegea na kuwa dhaifu zaidi hata inapofunguliwa au kutolewa nguo inayobana,”anasema. Kwa upande mwingine, mtaalamu wa misuli Dk Robert Shanks anasema kuwa nguo hizo zinachangia pia kusababisha maumivu ya mgongo kwa mvaaji. Anasema nguo hiyo inapovaliwa, kunakuwapo na ugumu kwa viungo vya mgongo kujongea kwa urahisi, hivyo kusababisha maumivu ya mgongo mara kwa mara. “Viungo na mifupa iliyopo kwenye mgongo inapaswa kujongea, lakini kuibana kupita kiasi kutasababisha kushindikana kwa hali hiyo hivyo mvaaji lazima atakumbana na maumivu ya mgongo mara kwa mara” Pamoja na madhara hayo, nguo hizi pia huweza kusababisha kizuizi katika mzunguko wa damu kwani mishipa inayotakiwa kufanyakazi hiyo inashindwa, kutokana na maeneo ya tumbo hadi kwenye nyonga yanakuwa yamebanwa. “Ni vigumu mzunguko wa damu kufanyika vizuri katika maeneo yaliyobanwa kupita kiasi; ni wazi kuwa nguo hizi siyo rafiki, huifanya damu isizunguke inavyopaswa,”anasema Dk Shanks na kuongeza: “Ikifikia hatua hiyo, kuna dalili mvaaji kuweza kupata maimivu ya miguu kwa kuwa mishipa ya damu iliyopo katika maeneo hayo inashindwa kufanya kazi yake vizuri.” Kwa upande wake mtaalamu wa masuala ya ngozi nchini Tanzania, Dk Isack Maro, anasema kuwa madhara yanayotokana na uvaaji huo siyo makubwa ikilinganishwa na ripoti ya utafiti unavyoeleza. “Inawezekana kukawapo uwezekeno wa kupata maradhi ya ngozi kutokana na mwili kubanwa kwa muda mrefu, hivyo jasho kushindwa kutoka na kutengeneza mazingira ya fangasi,”anasema Dk Maro na kuongeza: “Madhara yapo, lakini siyo kwa ukubwa huo. Inawezekana kuwakumba watu wachache mno kati ya wengi, lakini sidhani kama yanaweza kuwa kwa ukubwa huo.


CRISTIANO RONALDO!,RONALDO NDIYE MSHINDI WA TUZO YA BALLON D’OR

January 14, 2014

cristiano-ronaldo-a-remporte-le-ballon-d

Usiku wa jana jijini Zurich, FIFA imemtangaza nyota huyo raia wa Ureno kuwa mwanasoka bora wa dunia kwa mwaka 2013 ambayo itakuwa tuzo yake ya pili.
Cristiano Ronaldo amepata kura nyingi zaidi ya wapinzani wake Franck Ribéry na Leo Messi, kwa kushinda tuzo hiyo Ronaldo atakuwa ameusitisha ufalme wa Messi aliyekuwa ameishinda tuzo hiyo kwa miaka 4 mfululizo.
Chachu ya ushindi huo wa Ronaldo ni mabao 69 aliyofunga mwaka 2013, ikiwa ni pamoja na kuumaliza mwaka vizuri.
Ronaldo mwenyewe anajua kuwa ni mshindi tangu juma lililopita baada ya kudhibitisha kushiriki kwenye sherehe za tuzo hizo, pamoja na kushiriki Ronaldo amewapa mialika ndugu na rafiki zake wa karibu,mpenzi wake mwanamitindo Irina Shayak wakala wake Jorge Mendes.
Pia wapo viongozi mbali mbali wa Real Madrid akiwepo raisi Florentino Pérez, Emilio Butragueño, Zinedine Zidane na Sergio Ramos, ambaye ametangazwa kuwa beki bora wa kati sambamba na Mbrazil Thiago Silva.

Ballon-dOr-3019314 images2 re


NJIA KUMI KUSAIDIA KUPUNGUZA UNENE

January 2, 2014

1-ULAJI

Ipo mifumo miwili ya kula. Chakula unachokula na namna unavyokila.

Unavyokula.

-Kuna kula vyakula vidogo vidogo vyenye madini, vitamini, mafuta nk mara nyingi kwa siku; au kula milo michache (mmoja au miwili) mikubwa ili kujaza tumbo. Ulaji mdogo mdogo husaidia afya na kuingia mwilini vyema kuliko ulaji mkubwa wa mara chache. Tumbo lina musuli zinazofanya kazi kama mashine au mnyama. Gari likijaa sana hupata taabu kwenda. Punda hivyo hivyo. Ulaji mdogo mdogo unaosambazwa mara kadhaa kwa siku  ni bora maana mwili unachambua kila kitu kwa wepesi na haraka. Unapokula milo michache mikubwa unapalilia zaidi mafuta mwili.

(PENDEKEZO la kwanza.  Asubuhi, kunywa maji kwanza, matunda, kisha ndiyo chai na vitu vingine kama mkate au maandazi…)

-Wapo wanaodai kwamba wanakula matunda na mboga.

Tatizo ni kwamba mipangilio  yao huwa ya makosa. Mathalan wengi hula matunda baada ya chakula. Vimeng’enya  chakula (enzymes) tumboni hufanya kazi namna tofauti. Mathalan vile vinavyonyambua matunda ni tofauti na vinavyomeng’enya vitu vigumu zaidi kama nyama au wanga. Matunda hunyambuliwa haraka zaidi kuliko vyakula vingine. Hivyo ni bora kula matunda dakika10-20 kabla ya chakula. Ukila baadaye matunda hugeuzwa aina fulani ya pombe (fermented food) inayoelea tu juu ya chakula na kubakia kitu kingine badala ya kuingizwa haraka ndani ya damu kupitia utumbo mdogo, uwengu, moyo, ini, nk.

Tatizo jingine ni kupika sana mboga hadi zikapoteza nguvu.

-Mseto wa vyakula pia ni muhimu. Kwa mfano vyakula vyenye uchachu (“acid”) na vile vinavyomumunyuka haraka (“alkaline”) havitakiwi viliwe pamoja. Mfano ni matunda. Matunda chachu kama machungwa, mananasi na maembe yatakiwa yawe pamoja; na yale laini zaidi:  ndizi mbivu, matikiti maji, mapapai, matufaha, nk yaende kivyake, maana yana mfumo tofauti, wa kumeng’enywa.

Hali hiyo pia iko katika nyama. Nyama nyeupe (ndege na samaki) tofauti na nyama nyekundu (ng’ombe, kondoo, nk) ziliwe tofauti.

Chakula unachokula

Waafrika  hatuna tabia ya kula mboga mboga mbichi. Tunafuata ladha na mazoea kuliko thamani.

Bara letu lina mboga na vyakula bora kuliko bara lolote duniani lakini sisi tunakufa mapema na kwa utapia mlo kuliko wale wanaotoka nchi kame. Ulaya nzima imejazana mboga mboga zinazoagizwa toka Afrika. Kenya na Tanzania zinauza mboga za maharagwe mabichi (green beans), matunda toka Afrika Kusini na Ivory Coast; nk. Waafrika tunapenda kujaza matumbo. Unene umekithiri hata wale walio matajiri waliosoma bado wanakufa kwa kisukari shauri ya kutokula mboga mbichi.

Ulaji wa mboga mbichi ni upi?

Ni mathalani ulaji wa salad. Tanzania tunaita kachumbari. Lakini si lazima iwe kachumbari ya nyanya, vitunguu na chumvi tu. Waweza kuchanganya matango, nyanya kwa maparachichi; au vitunguu saumu, giligilani na karote. Huu mseto wa mboga mbichi ni mzuri ukienda na chakula chenye nyama za minofu na wanga (ugali, wali, ndizi za kupika nk). Ulaji wa wanga asubuhi, mchana na jioni kila siku huchangia sana katika unene.

(PENDEKEZO LA 2. Ugali kwa samaki; mboga ya majani ya matango kwa nyanya. Usiweke chumvi kwenye hiyo mboga mbichi ya majani.)

2-UNYWAJI  MAJI

Waafrika hatunywi maji, hasa wanawake. Wanaokunywa maji zaidi ni wacheza michezo. Wengi wetu hunywa zaidi soda (vinywaji baridi kama Cocacola, Pepsi, Mirinda ,Tangawizi  na gesi za kisasa kama Red Bull) zilizojaa gesi inayoleta vidonda tumboni; na chai. Kuliko maji. Na maji haya hutakiwa  dakika 10-20 kabla ya chakula au nusu saa kuendelea baada ya chakula. Ukila  chakula huku unasakatia maji huimanisha mtu una kiu. Ulaji chakula na unywaji maji ni vitu viwili tofauti. Ila utawaona watu wanakula huku wakibugia maji. Unapokula chakula huku unabugia maji unapunguza nguvu za chakula, unajaza tumbo maji na kuchelewesha mmeng’enyo wa chakula (digestion).

Chakula kisipomeng’enywa vizuri kinaketi tu tumboni. Matokeo wengi wetu tuna  matumbo makubwa. Kama hufanyi mazoezi lile tumbo linakwenda pembeni (chini ya mbavu) hasa kwa watu wa makamo linaleta maradhi kama kisukari, kiungulia, kuvimbiwa, uyabisi wa tumbo, nk. Kizungu huitwa “love handles.”…

3-SUALA LA UMENG’ENYAJI

Chakula huanza kumeng’enywa au kusagwa (kwa lugha iliyozoeleka) mdomoni. Mate yako mdomoni ni chanzo cha uchambuaji chakula. Unapobugia chakula bila kutafuna sawasawa unasababisha mambo mawili. Moja chakula kutochambuliwa vizuri, pili chakula kwenda kukaa tu tumboni, au kama kikipita hakisaidii lolote mwilini. Utafunaji wa taratibu husaidia umeng’enyaji. Chakula kinapofika tumboni hukaa pale dakika ishirini. Hapo huchanganywa na asidi (ya manjano iitwayo Hydrochloric) inayokibadilisha tayari kupelekwa utumbo mkubwa, kupitia kongosho. Kule uchafu utapelekwa chini na rutuba kusafirishwa na utumbo mdogo kuelekea katika uwengu, moyo. Moyo utadunda chakula kilichoshageuzwa damu kuelekea mwilini kufanya kazi na akiba hubakishwa katika ini.

Sasa kama usipotafuna vizuri, ukila huku unakunywa sana maji au vinywaji vingine chakula hakimeng’enywi vizuri. Ndiyo maana unawaona watu wengine wanakula sana lakini hawana afya. Wanaugua ovyo ovyo, wanatoka jasho ovyo, wanajamba ovyo, wana matumbo makubwa, wanavimbiwa, wanakaa siku nyingi bila kwenda choo (inatakiwa mtu kwenda haja kubwa mara moja au mbili kwa siku) nk.

4-ULAJI WA VYAKULA VYA MAFUTA

Mafuta ni suala muhimu sana mwilini. Ila ulaji wake shurti uwe wa mpangilio. Yaani unaowiana. Lazima mtu uwe na wastani mzuri wa vyakula vya nguvu, yaani “wanga” (ugali, ndizi, wali, viazi mbalimbali, mikate, mahindi, nk), ujenzi yaani “protini” (mboga na nyama), “madini” (mbegu mbegu mbichi si za kukaanga sana na chumvi) na “vitamini” (matunda, maziwa, mayai, nk).

Waafrika tunapenda nyama. Nyama ni muhimu sana maana ina madini aina ya chuma (nyama nyekundu) protini,nguvu na mafuta. Ila mafuta yaliyoko katika nyama mara nyingi si mazuri shauri hayatoki, huganda. Chukua nyama ya kuku na samaki ambayo huwa na ngozi. Wengi wetu hupenda sana kula ile ngozi ya wanyama hawa kwa kuwa tamu. Lakini haya ni mafuta mabaya.

Mafuta ya samaki lakini ni mazuri. Samaki anayo mafuta ya Omega-3 ambayo husaidia mwili na kinga maradhi mwilini.

Tunapokula nyama choma au ya kukaanga, lazima tule pia mboga za majani (mbichi) na si vizuri kula nyama kila siku. Kama huwezi kukaa bila nyama kila siku, fanya mazoezi ya mwili.

PENDEKEZO LA 3- Kula mbegu mbegu za korosho, karanga au mlozi (ziwe mbichi badala ya kukaanga na chumvi) kati kati ya siku. Haya ni mafuta yenye rutuba mwilini kuliko nyama za mafuta.

5-MAZOEZI YA MWILI NA VIUNGO

Mazoezi ni mfalme wa kupunguza unene.

Ukiwauliza wengi watakuambia wanafanya kazi ngumu za sulubu (wanachuruzikwa jasho) kwa hiyo hayo ni mazoezi. Ila kazi na mazoezi ni vitu viwili tofauti. Ingekuwa kufanya kazi ni mazoezi basi kusingekuwa na wastani mfupi wa maisha kwa maskini hasa sisi Waafrika.

Wengine watadai kwamba walipokuwa wadogo shuleni walifanya mazoezi sasa wamekuwa watu wazima (miaka 40 kuendelea) kwamba eti mazoezi ni suala la ujana; kumbe kadri unavyokuwa ki umri ndivyo kadri unavyotakiwa kufanya mazoezi na kujitazama zaidi kiafya.

Watazame Wachina na Wajapani wanavyoishi maisha marefu.

Mazoezi ni shughuli inayokufanya kwanza uheme (mapafu na moyo kwenda kasi), viungo na mifupa kujinyoosha (stretching), kutoka jasho na usafishaji wa damu. Mazoezi yanayosaidia haya ni pamoja na kutembea kasi, kukimbia, kuogelea, michezo mbalimbali ya riadha (kama mpira wa miguu, nyavu, kikapu, mikono, nk); michezo ya kupigana na kujilinda yaani masho ati(karate, kung fu, judo, capoeira, krav maga, jiu jitsu, systema, kickboxing, thai boxing, kempo, kalari payatu, aikido, nk) …

Ni muhimu mwanadamu ufanye mazoezi makali ya viungo mara mbili tatu kwa juma. Si vizuri kufanya kila siku kwani musuli na mishipa inahitaji kupumzika na kukua.

Kama unapenda kuinua vyuma lazima uwe na mwalimu wa kukuelekeza; na si vizuri kufanya kila siku.  Wastani wa mara mbili tatu kwa juma inatosha kabisa.

6-UPO UFANYAJI MAZOEZI WA AINA MBILI

Mazoezi ya nguvu ya kuhema niliyotaja hapo juu (cardio-vascular) na yale laini ya kujinyoosha yaani ambayo hutumia zaidi nguvu za ndani na pumzi. Haya ya pili ni kama Yoga (India) , Tai Chi Chuan (China) na aina mpya mazoezi iliyoanza Majuu miaka ya karibuni yaani Pilates (hutamkwa hivyo hivyo ilivyoandikwa Pilates). Haya laini yanawafaa zaidi watu wazima na nchini China na Japan mathalan utawakuta wazee wa miaka 80 hadi 90 bado wanayafanya. Husaidia moyo, damu na akili.

Michezo na mazoezi ya mwili ni njia kuu ya kupunguza unene, kurefusha maisha, kuchangamsha ubongo, kupunguza ulevi, uvutaji sigara, dawa za kulevya, tabia mbaya za uvivu, ugomvi, nk.  Mataifa yenye watu wanaofanya mazoezi kama Japan, Brazili, India, China nk  huwa na wachapa kazi wengi na wananchi wanaoipenda jamii yao.

7-KULA SANA CHUMVI SI VIZURI

Ulaji chumvi mwingi hutokana na suala la ladha. Kisayansi vyakula  vyote vina chumvi asilia sema tu tumezoea kuongezea madini hii iitwayo Sodium. Sodium inachangia sana kufupisha maisha. Huifanya mishipa ya damu ichoke; ni kama bomba lolote la maji ukilitazama baadaye hugeuka rangi kutokana na yale maji kupita pale kila siku.

Kwa wale tunaoishi nchi za joto na kutoka sana jasho kula chumvi ni muhimu. Ila tatizo letu ni kwamba hatunywi maji ya kutosha. Mtu ukiwa na kiu unakunywa soda au kinywaji cha sukari; inakuwa kama unaendelea kuutesa mwili. Kwa vipi? Mishipa inayopitisha damu mwilini badala ya kusaidiwa kwa maji inawekewa kazi zaidi ya kusafisha sukari na chumvi. Ndiyo maana vifo vingi vinatokea mapema; wastani wetu wa maisha haupiti miaka 50.

Utafiti uliofanywa chuo kikuu cha California, Marekani mwanzoni mwa 2010, umethitibisha kwamba vifo vingi duniani husababishwa na maradhi ya moyo na saratani ambavyo hutokana na uvutaji sigara, unene, ulevi na ulaji sana wa chumvi na sukari. Tukipunguza ulaji wa chumvi tunasaidia pia kupunguza maradhi ya moyo, utafiti unasema.

8-TAFITI ZA VYUO KADHAA ULIMWNGUNI KUHUSIANA NA AFYA

-Jarida la Kimarekani la sayansi lilieleza mwaka jana kwamba utapunguza ugonjwa wa moyo (ambao husababishwa na unene , wasiwasi na purukshani) kwa asilia mia 42 kama utakula matunda na mboga za majani peke yake kila siku, juu ya msosi wa kawaida.

(PENDEKEZO LA KULA- Na 4- Kula mlo wako. Baada ya saa mbili au tatu, sakatia tunda au matunda; baada ya mlo mwingine, kula sahani ya mseto wa mboga mbichi kama karote na matango. Utaona tofauti ya afya, ngozi, wajihi, kinyesi, usingizi, nk. Kidesturi tumezoea kunywa chai au soda za sukari sukari na gesi kati kati nya milo badala ya matunda na mboga mbichi za majani).

-Utafiti uliofanywa na wanasayansi  chuo kikuu cha South Carolina mwanzo wa mwaka 2010 kuhusu faida za kuogelea.

Zoezi la kuogelea  lina faida zaidi ya kukimbia au kutembea kwa vile huchanganya mazoezi makali na pumzi, kusaidia mapafu na moyo. Utafiti ulithibitisha kuogelea hupunguza hatari za kifo kwa asili mia hamsini.

-Utafiti wa jarida la chuo cha uganga Ulaya umeeleza (desemba 2009) kwamba kulala nusu saa kila mchana (“nap”) husaidia  kupunguza ugonjwa wa moyo kwa asilimia 37.

-Uchunguzi wa chuo cha michezo cha Hispania mwanzoni mwa 2010 umethibitisha kwamba ukikimbia mara tatu kwa juma (jogging) unaongeza nyege mwilini kwa asili mia 75. Hasa kwa watu wa makamo mnaoanza kupoteza nguvu za urijali.

-Uchunguzi chuo kikuu cha Leeds, Uingereza  mwanzoni mwa 2010 umeonyesha unapotembea kwa miguu, ukikwepa barabara kubwa zisisokuwa na mioshi ya magari (pollution) unapunguza matatizo ya maradhi ya hewa chafu kama pumu, mapafu na appendix.

-Uchunguzi wa chuo kikuu cha Texas mwaka 2010 umegundua kwamba  kula tunda la divai nyekundu mara kwa mara husaidia kupunguza  kupata ugonjwa wa kisukari.

-Hapo hapo tunaelezwa kwamba watu weusi na bara la Asia wanakumbwa zaidi na ugonjwa wa kisukari kutokana na vinywaji vya sukari sukari na gesi (fizzy drinks). Ukinywa kiasi cha miligramu 300 za vinywaji hivi (Cocacola, Red Bull, Fanta, nk)  kwa siku unajitahadharisha kupata kisukari.

9-KUFUNGA

Neno kufunga linatambuliwa rasmi kuhusiana na Waislamu (mwezi Ramadhani) au Wakristo (Lenti nk). Ufungaji huo una masharti mengine ya kidini tofauti na haya ya kiafya.

Mathalani wafungaji  hawa hula chakula kingi usiku; ukihesabu wanafunga wastani wa saa 12 tu. Kawaida ukitaka virusi na takataka nyingine mwilini zitoweke, au viungo vipumzike wahitaji saa 20 kuendelea.

Ufungaji ninaouongelea ni ufungaji wa kutokula kabisa kwa saa 24, 36 hadi 48 kuendelea…

Ufungaji ni nini?

Kama mashine yeyote mwili wa mwanadamu unahitaji kupumzika na kujisafisha. Hata tukiwa tumelala bado viungo mbalimbali mwilini vinafanya kazi. Kwa hiyo faida ya kwanza kabisa ya kufunga ni kuupumzisha mwili kama mfanyakazi yeyote anapokwenda likizo.

Faida ya pili ya kufunga ni kusafisha mwili kutokana na uchafu ambao haukutoka (kinyesi hakitoi mabaki yote toka utumbo mkubwa), dawa na takataka za mazingira tunayoyavutia hewa, virusi au kuyanywa katika maji na vyakula mbalimbali na pia uchafu wa hisia, yaani hasira, huzuni, nk.

Kuna ufungaji wa aina mbalimbali.

1-Kufunga kwa kunywa maji tu, saa 24 kuendelea…

2-Kufunga kwa kutokunywa maji au kula chochote, saa 24 kuendelea…

3-Kufunga kwa kula tu matunda au mboga zilizopondwa kama karote, matango nk, saa 24 kuendelea…

Ufungaji huu unatakiwa ufanywe kwa mpangilio. Kitu muhimu si tu kufunga bali NAMNA unavyofungua. Ukianza kula tena, unaanza taratibu. Kawaida ni vizuri kuanza na maji, kikombe au bilauri ya kwanza taratibu. Subiri tena nusu saa, bilauri nyingine, halafu hadi ya tatu, halafu ndiyo matunda yasiyo ya chachu, na kadhalika. Kuanza kufungua kwa kunywa chai ya maziwa, uji au vyakula vingine vya wanga hakusadii sana mfungo huu.

Maana lengo lake ni kusafisha mwili.

PENDEKEZO LA 5- Kwa wenye imani za kidini. Unaweza pia kufunga hivi ukawa pia unasali au kuvaa mavazi yanayokufanya mtu wa amani. Ukifanya hivi unajitakasa kimwili na kiroho. Si lazima ungojee ile miezi ya kufunga na wengine.

10-USINGAJI

Usingaji au masaji ni njia nzuri sana ya kupunguza unene. Ikiwa unaangalia namna unavyokula, unafanya mazoezi na kusingwa mara moja au mbili kwa mwezi unaupalilia mwili vizuri. Nini faida ya usingaji? Kusinga husaidia ngozi, mishipa ya damu na sura nzima ya mwili na taswira yako mwanadamu. Wengi wetu tunaposikia neno kusinga tunafikiria usingaji wa mapenzi. Hivi ni vitu viwili tofauti kwani usingaji wa mapenzi unaimanisha mahusiano ya kihisia.

Kifupi mwanadamu unatakiwa uwe unautunza na kuungalia mwili wako kama nyumba au hekalu lako. Wengi wetu tunaoga, tunajipaka marashi, tunasuka, tunanyoa nywele au ndevu; lakini miili yetu kiundani inaoza taratibu…

Kama alivyosema mpiganaji, msanii, mwanafalsafa, mwigizaji, mwandishi mashuhuri marehemu Bruce Lee katika shairi  lake Mazingira Yako Kimya (toka kitabu “Msanii wa Maisha”, Turtle Publishing, 2001):


FAIDA YA JUISI YA UKWAJU

January 2, 2014

1) Chanzo kizuri cha viuasumu mwilini ‘antioxidants’ ambavyo huzuia Saratani (cancer)
2) Chanzo cha Vitamini B na C vile vile “carotentes”
Hushusha joto la mwili na kuondosha homa, h asa homa ya malaria na homa ya matumbo
3) Huulinda mwili dhidi ya mafua na kero za mafua kooni
Husaidia myeyusho na mmengenyo wa chakula na kuondosha kuvimbiwa
4) Husaidia kutibu matatizo ya nyongo (bile disorders)
5) Husaidia kurahisisha choo (laxative)
6) Husaidia kupunguza wingi wa lehemu (cholesterol) na hivyo kuimarisha moyo
7) Husaidia ngozi kuwa nyororo, vile vile husaidia ngozi inayopona baada ya kuungua au yenye vidonda
8) Husaidia kuua minyoo tumboni (kwa watoto wadogo)
9) Husaidia ngozi kuwa nyororo, vile vile husaidia ngozi inayopona baada ya kuungua au yenye vidonda
10) Husaidia kuua minyoo tumboni (kwa watoto wadogo)

Jinsi ya Kuwa na Ndoa Yenye Mafanikio

January 2, 2014

NDOA inaweza kufananishwa na safari ndefu yenye matukio yasiyotazamiwa, mengine yenye kupendeza na mengine yenye kuumiza. Hali zisizotazamiwa zinaweza kutokeza vizuizi visivyotarajiwa, vingine vikionekana kuwa vikubwa sana. Hata hivyo, watu wengi humaliza safari hiyo kwa furaha na mafanikio, wakiwa wamekabili matatizo madogo tu. Kwa kweli, mafanikio katika ndoa hayapimwi kwa panda shuka za safari bali yanapimwa kwa jinsi wenzi wanavyoshughulikia hali hizo.

Unafikiri ni nini kinachoweza kufanya safari ya ndoa ifanikiwe zaidi na iwe yenye kufurahisha? Wenzi wengi wanaona uhitaji wa kuwa na ‘ramani ya ndoa’ ili iwaelekeze njiani. “Ramani” inayotegemeka na yenye mamlaka kuhusu ndoa imeandaliwa na Mwanzilishi wa ndoa—Yehova Mungu. Hata hivyo, Neno lake lililoongozwa na roho, Biblia Takatifu, si hirizi. Badala yake, lina mwelekezo unaofaa ambao wenzi waliooana wanapaswa kufuata ili ndoa yao ifanikiwe.—Zaburi 119:105; Waefeso 5:21-33; 2 Timotheo 3:16.

Acheni tuone baadhi ya alama za Kimaandiko za kuonyesha njia, yaani, kanuni muhimu za Biblia ambazo zinaweza kukuongoza katika safari ya ndoa yenye furaha na mafanikio.

Ione ndoa kuwa takatifu. “Kile ambacho Mungu ameunganisha mtu yeyote asikitenganishe.” (Mathayo 19:6) Muumba alianzisha mpango wa ndoa alipomleta Hawa kwa mwanamume wa kwanza, Adamu. (Mwanzo 2:21-24) Kristo Yesu, ambaye alishuhudia tukio hilo alipokuwa mbinguni alithibitisha kwamba muungano wa Adamu na Hawa katika ndoa ulipaswa kudumu. Alisema: “Je, hamkusoma kwamba yeye aliyewaumba hao kutoka mwanzo aliwafanya mwanamume na mwanamke na kusema, ‘Kwa sababu hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye atashikamana na mke wake, na hao wawili watakuwa mwili mmoja’? Hivi kwamba wao si wawili tena, bali mwili mmoja. Kwa hiyo, kile ambacho Mungu ameunganisha mtu yeyote asikitenganishe.”—Mathayo 19:4-6.

Kwa kusema “kile ambacho Mungu ameunganisha,” Yesu hakuwa akidokeza kwamba Mungu hupanga ndoa mbinguni. Badala yake, alikuwa akithibitisha kwamba uhusiano wa ndoa ulianzishwa na Mungu mwenyewe na hivyo ulipaswa kuonwa kuwa mtakatifu.*

Bila shaka, waume na wake hawangependa ‘kuunganishwa’ katika uhusiano usio na upendo. Badala yake, wanataka kufurahia ndoa yenye kuridhisha itakayowaimarisha. Wanaweza ‘kuunganishwa’ kwa furaha ikiwa watafuata mashauri ya Muumba yanayopatikana katika Biblia.

Kwa sababu sisi sote si wakamilifu, hatuwezi kuepuka kutoelewana na kutopatana. Hata hivyo mara nyingi, ndoa yenye mafanikio haitegemei kufaana kwa wenzi wa ndoa, bali inategemea jinsi wanavyokabiliana na mambo ambayo hawapatani. Hivyo, mbinu moja muhimu sana katika ndoa ni uwezo wa kusuluhisha mambo kwa upendo, kwa kuwa upendo “huunganisha kila kitu katika umoja ulio kamili.”—Wakolosai 3:14, Biblia Habari Njema.

Zungumza kwa heshima. “Kuna mtu anayesema bila kufikiri kama kwa upanga unaochoma, lakini ulimi wa mwenye hekima huponya.” (Methali 12:18) Wachunguzi wamegundua kwamba mazungumzo mengi huisha vile yalivyoanza. Kwa hiyo, ikiwa mazungumzo yanaanza kwa heshima, kuna uwezekano mkubwa kwamba yatamalizika vivyo hivyo. Kwa upande mwingine, unajua jinsi unavyoumia mpendwa anapokuambia jambo bila kufikiri. Hivyo, sali na ujitahidi kuzungumza kwa staha, heshima, na upendo. (Waefeso 4:31) “Hata ingawa kila mmoja huona udhaifu wa mwenzake,” anaeleza Haruko,* mwanamke Mjapani ambaye amekuwa katika ndoa kwa miaka 44, “tunajitahidi kuheshimiana kwa maneno na mtazamo. Hilo limetusaidia kuwa na ndoa yenye mafanikio.”

Sitawisha fadhili na huruma. “Iweni wenye fadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma nyororo.” (Waefeso 4:32) Kunapokuwa na ugomvi mkali, mara nyingi mwenzi mmoja akikasirika yule mwingine hukasirika pia. Huko Ujerumani, Annette, ambaye amekuwa katika ndoa yenye furaha kwa miaka 34 anakiri hivi: “Si rahisi kuwa mtulivu chini ya mfadhaiko—inaelekea utasema mambo yatakayomkasirisha mwenzi wako, na kufanya hali iwe mbaya hata zaidi.” Hata hivyo, kwa kujitahidi kuwa mwenye fadhili na huruma, unaweza kuchangia sana katika kunyoosha njia ya kupata ndoa yenye amani.

Onyesha unyenyekevu. ‘Usifanye jambo lolote kwa ugomvi au kwa kujisifu, bali kwa unyenyekevu wa akili ukiwaona wengine kuwa ni bora.’ (Wafilipi 2:3) Ugomvi mwingi hutokea kwa sababu badala ya kujinyenyekeza na kutafuta njia za kuboresha hali, kiburi huwafanya watu walaumu wenzi wao matatizo yanapotokea katika ndoa. Unyenyekevu wa akili unaweza kukusaidia usisisitize kwamba wewe ndiye uko sawa ugomvi unapotokea.

Usiudhike haraka. “Usiwe na haraka kuudhika katika roho yako.” (Mhubiri 7:9) Jaribu kuepuka mwelekeo wa kupinga maoni ya mwenzi wako au kujitetea haraka mwenzi wako akikuuliza kuhusu jambo ulilosema au kufanya. Badala yake, sikiliza maoni ya mwenzi wako. Fikiria kwa uangalifu kabla ya kujibu. Watu wengi hujifunza wakiwa wamechelewa mno kwamba kuwa na uhusiano wenye upendo na wenzi wao ni muhimu kuliko kushinda mabishano.

Jua wakati wa kukaa kimya. ‘Uwe mwepesi kuhusu kusikia, si mwepesi wa kusema, si mwepesi wa ghadhabu.’ (Yakobo 1:19) Bila shaka, mawasiliano mazuri ni mojawapo ya ishara muhimu sana katika barabara inayoelekeza kwenye ndoa yenye furaha. Kwa nini basi Biblia inasema kwamba kuna “wakati wa kukaa kimya”? (Mhubiri 3:7) Huenda huo ukawa wakati wa kusikiliza kwa makini ili uelewe anachosema mwenzi wako, na hiyo ni sehemu muhimu ya mawasiliano inayotia ndani kujua hisia za mwenzi wako wa ndoa na kwa nini anahisi hivyo.

Onyesha hisia-mwenzi unaposikiliza. “Shangilieni pamoja na watu wanaoshangilia; lieni pamoja na watu wanaolia.” (Waroma 12:15) Hisia-mwenzi ni muhimu ili kuwasiliana inavyofaa kwa sababu inakuwezesha kuhisi hisia za ndani kabisa za mwenzi wako. Sifa hiyo inawezesha kuwe na hali ambayo maoni na hisia za kila mmoja zinaheshimiwa. Nella kutoka Brazili ambaye amekuwa katika ndoa kwa miaka 32 anasema hivi: “Tunapozungumzia matatizo yetu, mimi husikiliza kwa makini ili nielewe mawazo na hisia za Manuel.” Mwenzi wako anapozungumza, huo ni “wakati wa kukaa kimya” na kumsikiliza ukionyesha hisia-mwenzi.

Uwe na zoea la kuonyesha uthamini. “Mjionyeshe kuwa wenye shukrani.” (Wakolosai 3:15) Waume na wake katika ndoa imara huhakikisha kwamba wenzi wao wanajua jinsi wanavyowathamini. Hata hivyo, kwa sababu ya pilka-pilka za kila siku katika ndoa, watu fulani wamepuuza sehemu hiyo muhimu ya mawasiliano na kudhani kwamba wenzi wao wanajua wanathaminiwa. “Wenzi wengi,” anasema Dakt. Ellen Wachtel, “wangeweza kuonyeshana uthamini ikiwa wangekumbuka kufanya hivyo.”

Wake hasa wanahitaji kuhakikishiwa kwa upendo na kuonyeshwa na waume wao kwamba wanathaminiwa. Waume, mnaweza kufanya mengi kuboresha ndoa yenu na hali njema ya wake wenu na yenu wenyewe kwa kuwa na zoea la kuwapongeza wake wenu kwa sababu ya matendo mazuri na sifa zao.

Ni muhimu kumhakikishia hivyo kwa maneno na kwa matendo. Mume, unapombusu mke wako, kumgusa kwa wororo, na kutabasamu kwa uchangamfu, mambo hayo yanatimiza mengi zaidi ya kumwambia “nakupenda.” Kufanya hivyo kunamhakikishia kwamba yeye ni mwenye thamani kwako na unamhitaji. Mpigie simu au umwandikie ujumbe mfupi kwa simu ukimwambia, “ninakukosa” au ukimwuliza “Siku yako inaendeleaje?” Ikiwa umeacha mazoea hayo ambayo ulikuwa nayo mlipokuwa mkichumbiana, ingefaa uanze tena. Endelea kutafuta ni nini kinachomgusa moyo.

Maneno haya ya mama ya Mfalme Lemueli wa Israeli la kale yanafaa: “Mumewe huimba sifa zake. Husema, ‘Wanawake wengi wametenda mambo ya ajabu, lakini wewe umewashinda wote.’” (Methali 31:1, 28, 29, BHN) Wewe ulimsifu mke wako lini mara ya mwisho? Au ikiwa wewe ni mke, ulimsifu mume wako lini?

Uwe mwenye haraka kusamehe. “Jua lisitue mkiwa katika hali ya kuchokozeka.” (Waefeso 4:26) Ukiwa katika ndoa, wewe na mwenzi wako hamwezi kuepuka kufanya makosa. Hivyo, kuwa tayari kusamehe ni muhimu. Clive na Monica, huko Afrika Kusini, ambao wameoana kwa miaka 43, wameona shauri hili la Biblia kuwa lenye kusaidia sana. Clive anaeleza hivi: “Sisi hujaribu kutumia kanuni inayopatikana katika Waefeso 4:26, nasi hujaribu kusameheana haraka, kwa kuwa tunajua kwamba hilo humpendeza Mungu. Baada ya hapo, sisi hulala vizuri kwa kuwa tuna dhamiri safi.”

Methali ya kale inasema hivi kwa hekima: ‘Ni jambo lenye kupendeza kupita kosa.’ (Methali 19:11) Annette, aliyetajwa awali, anakubaliana na hilo, naye anaongezea: “Hamwezi kuwa na ndoa nzuri ikiwa hamsameheani.” Anaeleza sababu: “Msiposameheana, mtakuwa na kinyongo na kutoaminiana, na mambo hayo ni sumu kwa ndoa. Mnaposameheana, kifungo cha ndoa huimarishwa na mnakuwa na uhusiano wa karibu sana.”

Unapomuumiza mwenzi wako kihisia, usikate kauli kwamba atakusamehe na kusahau. Mara nyingi, kufanya amani kunahusisha mojawapo ya mambo magumu kwa wenzi wa ndoa: Kukubali kwamba umefanya makosa. Tafuta njia za kusema hivi kwa unyenyekevu: “Naomba radhi, mpenzi. Nilikosea.” Kuomba msamaha kwa unyenyekevu kutafanya uheshimiwe, uaminiwe, na uwe na amani ya akili.

Uwe mwaminifu kwa mwenzi wako na kwa ndoa yako. “Wao [mume na mke] si wawili tena, bali mwili mmoja. Kwa hiyo, kile ambacho Mungu ameunganisha mtu yeyote asikitenganishe.” (Mathayo 19:6) Wewe na mwenzi wako mliweka nadhiri nzito mbele za Mungu na watu kwamba mtaishi pamoja, chini ya hali zozote zile.* Hata hivyo, kutimiza wajibu katika ndoa hakuhusishi kutimiza matakwa ya kisheria tu. Badala yake, mtu anapaswa kuchochewa na upendo wa kutoka moyoni, na hilo litaonyesha kwamba anamheshimu na kumstahi Mungu na pia mwenzi wake. Kwa hiyo, usidhoofishe ndoa yako takatifu kwa kucheza-cheza na wengine kimapenzi; pendezwa kimahaba na mwenzi wako tu.—Mathayo 5:28.

Kujidhabihu kunaimarisha ushikamanifu. ‘Endelea kuangalia, si faida za kibinafsi za mambo yako mwenyewe tu, bali pia faida za kibinafsi za wengine.’ (Wafilipi 2:4) Kutanguliza mahitaji na mapendezi ya mwenzi wako ni njia moja ya kuimarisha ushikamanifu wako. Premji, ambaye amekuwa katika ndoa kwa miaka 20, humsaidia kazi za nyumbani mke wake ambaye anafanya kazi ya kuajiriwa. “Mimi humsaidia Rita kupika, kusafisha, na kazi nyingine ili awe na wakati na nguvu za kufanya mambo anayopenda.”

Jitihada Zinathawabisha

Nyakati nyingine, huenda kazi ngumu inayohusika ili kuwa na ndoa yenye furaha ikafanya watu fulani watake kukata tamaa. Hata hivyo, usiache matatizo yakufanye uache kutimiza wajibu au utupilie mbali jitihada ambazo umefanya kufikia sasa kufanikisha ndoa yako, yaani, usikatize safari yako ya kuwa na ndoa yenye mafanikio.

“Ukijitahidi vilivyo na kuonyesha kwamba unataka ndoa yako ifanikiwe, utapata baraka za Yehova,” anasema Sid, ambaye ndoa yake imefanikiwa kwa miaka 33. Mkitegemezana kwa ushikamanifu nyakati za shida na mkifurahia pamoja nyakati za shangwe mtadumu katika safari yenye kuridhisha ya kuwa na ndoa yenye mafanikio.

[Maelezo ya Chini]

Yesu alisema kwamba msingi pekee wa kuvunja ndoa na kuwa huru kuoa au kuolewa tena ni uasherati, yaani, ngono nje ya ndoa.—Mathayo 19:9.

Baadhi ya majina katika makala hii yamebadilishwa.

Biblia inampa mwenzi asiye na hatia haki ya kuamua ikiwa atamtaliki mwenzi aliyefanya uzinzi. (Mathayo 19:9) Ona makala “Maoni ya Biblia: Uzinzi—Kusamehe au Kutosamehe?” katika Amkeni! la Agosti 8, 1995 (8/8/1995).

[Blabu katika ukurasa wa 6]

Biblia ni kama ramani ya kutuongoza katika safari ya ndoa

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

Mnapohitaji kuzungumzia tatizo fulani

Pangeni kufanya hivyo wakati hamjachoka.

Epukeni kuchambuana na muwe na mtazamo unaofaa.

Epuka kumkatiza mwenzako anapoongea; kila mmoja awe na zamu ya kusikiliza na kuongea.

Tambua hisia za mwenzi wako.

Onyeshaneni hisia-mwenzi, hata msipokubaliana.

Muwe na usawaziko na tayari kubadilikana.

Omba msamaha kwa unyenyekevu unapokosea.

Onyeshaneni uthamini na upendo.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

Ili ndoa ifanikiwe

Zingatia kweli za Biblia ambazo huimarisha ndoa.

Tafuta wakati kwa ajili ya ndoa na mwenzi wako.

Uwe mchangamfu, mwenye upendo, na urafiki.

Uwe mwenye kuaminika na mshikamanifu.

Onyesha fadhili na heshima.

Saidia kazi za nyumbani.

Jitahidi kuwa na mazungumzo yenye kufurahisha.

Iweni na ucheshi na tafrija pamoja.

Endeleeni kujitahidi kuimarisha ndoa yenu.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]

Mambo ya kutafakari kibinafsi

Ninahitaji kufanyia kazi nini katika ndoa yangu?

Nitachukua hatua gani kufanya hivyo?


%d bloggers like this: